Saturday 7 May 2016

UJENZI WA NYUMBA KWA KUTUMIA MATOFALI YANAYOFUNGAMANA (INTERLOCKING BLOCKS)


 Mwendelezo wa toleo lililopita.............
Ujenzi wa nyumba umegawanyika katika hatua zifuatazo: -

      Kupima msingi wa jengo
 
   
      Kuchimba msingi
      Kumwaga zege la msingi
      Kujenga kuta za msingi
      Kuweka kifusi na kushindilia
      Kupanga mawe
      Kumwaga zege la jamvi
      Kujenga kuta za boma
      Kumwaga zege la linta
      Kujenga juu ya linta
      Kupaua jengo
      Kuweka milango na madirisha
      Kazi za umaliziaji na kazi za huduma mbalimbali mfano; umeme, maji, simu n.k
 
Ujenzi wa ukuta wa msingi

     Ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu wakati wa utengenezaji wa tofali za msingi kuhusu uchanganyaji wa udongo na saruji. Vipimo vya unene vya ukuta wa msingi na kina hutegemea na aina ya jengo na sifa za udongo uliopo, inashauriwa kina kisiwe chini ya sentimeta 45 na unene wa ukuta wa msingi usiwe chini ya sentimeta 30 (urefu wa tofali moja).


 
Kuseti kuta za boma
     Hatua inayofuata ni kuseti kuta za boma kwa kutumia ramani iliyopo. Hatua hii hufanyika kwa namna mbili: kwanza ni kuyapanga matofali kwa kuzingatia vipimo vya urefu wa kuta na kuondoa tofali maeneo yote ya uwazi kama milango na maeneo ya wazi ambayo yana mwendelezo wa ujenzi baada ya linta. Vipande robo tatu tofali hutumika wakati wa kugawa vyumba na kwenye maungio msalaba

 


Kujenga kuta za boma

    Tofali huunganishwa kwa udongo mwashi kwenye kitako (bed jointing). Ni muhimu kutumia udongo mwashi kwenye kozi ya kwanza ili kuweka muunganiko kati ya sehemu ya chini ya nyumba(substructure) na ile ya juu (superstructure). Katika hatua hii ni lazima kuhakikisha kuwa kuta zinanyooka na zina pimamaji. Ikumbukwe kuwa kuanzia kozi ya 2 hadi kwenye ring beam tofali hujengwa bila kutumia udongo saruji. Hata hivyo, kwa ajili ya kuongeza uimara udongo saruji laini (1:3) huwekwa kwenye kona, kwenye makato ya milango na madirisha. Kozi ya 2, kwa kuta za kugawa vyumba unaanza na tofali mbili za robo tatu ili kuondoa mfuatano wa maungio wima(straight vertical joints).
    Vipande vya nusu tofali hutumika zaidi kwenye makato ya madirisha na milango ili kuondoa mfuatano wa maungio wima.

 


Kutengeneza na kufunga boksi

    Utengenezaji wa box hufanyika kwa kuunganisha kwanza mbao za pembeni, kwa kutumia vibao maalum na kisha kulipachika ukutani na kuunganishwa na mbao za sahani kwa kutumia misumari. Box ni lazima liimarishwe vizuri pamoja na kuweka mirunda sehemu zote stahiki ili kuzuia kupinda au kuyumba kwa box hilo wakati wa kuweka zege.

 
   Ujenzi wa matofali mfereji (channel blocks)

    Hii ni teknolojia ambayo hupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mbao/miti kama vifaa vya kutengeneza kalibu ya kushika zege laini, ambapo matofali yenye umbo la kalibu hujengwa juu ya mstari wa mwisho kabla ya linta kwa lengo la kupokea zege laini. Kwa kuwa matofali hayo hufanana na tofali nyingine huficha eneo lenye linta na kufanya nyumba ionekane vizuri (Disappearing formwork).
    Hapa matumizi ya mbao za sahani na mirunda ni kwenye madirisha, milango na maeneo mengine yaliyo wazi, ambapo kuna linta. Njia hii ni bora, rahisi na rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya miti/mbao.
 


Kumwaga zege la linta
    Kabla ya kumwaga zege ni bora kufanya yafuatayo kwanza; kuweka nondo, kuweka nyaya za kufungia wall plates na kuweka mabomba ya umeme (conduit pipe) kwa nyumba yenye huduma ya umeme. Pia vipande vya mbao vyaweza kutumika kuweka matundu kwenye zege na kuvitoa zege likishanyauka kwa ajili ya kupitisha bomba za umeme pale ambapo kazi ya umeme itafanyika baadae na si lazima kununua bomba kipindi hicho kazi ya kumwaga zege ni kama inavyofanyika kwenye ujenzi wa kawaida isipokuwa tu, ni lazima kuhakiki kuwa mabomba ya umeme yako wima.
Ujenzi wa tofali juu ya linta
    Kozi ya kwanza baada ya linta, udongo mwashi hutumika ili kuunganisha linta na ukuta wa juu. Pia kulingana na ramani ukuta wa hanamu (gable) hujengwa baada ya kukamilika kwa hizo kozi 4. Ni muhimu matundu ya tofali kwa kuta zilizopo juu ya linta yajazwe udongo saruji laini.

 
 

2 comments: