Monday 9 May 2016

IJUE MAABARA YA KUPIMA VIFAA VYA UJENZI YA NHBRA

Maabara ya NHBRA imegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni:
  • Wet laboratory
  • Dry laboratory
Lengo la kupima ubora au uimara wa vifaa vya ujenzi au kufanya majaribio mbalimbali katika maabara ni kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika kwa ujenzi vinafikia kiwango cha chini cha ubora unaohitajika (minimum quality/strength requirement) kilichowekwa.


Oven
MAJARIBIO MBALIMBALI:

Majaribio ya udongo (soil test)
  • Kupambanua aina za udongo (soil classification)
  • Kushindilia (compaction related tests)
  • Upitishji maji na Uimara (compressibility, permeability and durability tests)
  • Jaribio la eneo la kazi (in-situ tests)
  • Shear strength tests
  • 
    Mashine ya kupima uimara wa udongo
Matofali na zege (blocks, bricks and concrete)
  • Mkandamizo (compressive strength)
  • Mchanganyiko (concrete mix design)
  • Kunyonya maji (absorption test)
  • Rebound hammer
  • Slump test
  • 
    Mashine ya kupima uimara wa zege na matofali
Aggregates
  • Kusagika (aggregates crushing value)
  • Kupondeka (aggregates impact value)
  • Kunyonya maji (water absorption)
  • Uimara kwenye msuguano (Los Angels abrasion value)
  • Uzito (bulk density)
  • Mabaki ya mimea (organic impurities)
Nondo
  • Kuvutika (Tensile strength)
  • Kukunjika (bending test)
  • Kukunjuka/kukunjua (rebending test)
Mbao (timber)
  • Unyevunyevu (moisture content)
  • Kukunjika (bending test)
Nachukua nafasi hii kuwakaribisha nyote kutumia maabara hii ambayo imesheheni na vifaa vya kisasa kwa vipimo na majaribio mbalimbali ya masuala ya ujenzi. nyote mnakaribishwa.

Saturday 7 May 2016

UJENZI WA NYUMBA KWA KUTUMIA MATOFALI YANAYOFUNGAMANA (INTERLOCKING BLOCKS)


 Mwendelezo wa toleo lililopita.............
Ujenzi wa nyumba umegawanyika katika hatua zifuatazo: -

      Kupima msingi wa jengo
 
   
      Kuchimba msingi
      Kumwaga zege la msingi
      Kujenga kuta za msingi
      Kuweka kifusi na kushindilia
      Kupanga mawe
      Kumwaga zege la jamvi
      Kujenga kuta za boma
      Kumwaga zege la linta
      Kujenga juu ya linta
      Kupaua jengo
      Kuweka milango na madirisha
      Kazi za umaliziaji na kazi za huduma mbalimbali mfano; umeme, maji, simu n.k
 
Ujenzi wa ukuta wa msingi

     Ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu wakati wa utengenezaji wa tofali za msingi kuhusu uchanganyaji wa udongo na saruji. Vipimo vya unene vya ukuta wa msingi na kina hutegemea na aina ya jengo na sifa za udongo uliopo, inashauriwa kina kisiwe chini ya sentimeta 45 na unene wa ukuta wa msingi usiwe chini ya sentimeta 30 (urefu wa tofali moja).


 
Kuseti kuta za boma
     Hatua inayofuata ni kuseti kuta za boma kwa kutumia ramani iliyopo. Hatua hii hufanyika kwa namna mbili: kwanza ni kuyapanga matofali kwa kuzingatia vipimo vya urefu wa kuta na kuondoa tofali maeneo yote ya uwazi kama milango na maeneo ya wazi ambayo yana mwendelezo wa ujenzi baada ya linta. Vipande robo tatu tofali hutumika wakati wa kugawa vyumba na kwenye maungio msalaba

 


Kujenga kuta za boma

    Tofali huunganishwa kwa udongo mwashi kwenye kitako (bed jointing). Ni muhimu kutumia udongo mwashi kwenye kozi ya kwanza ili kuweka muunganiko kati ya sehemu ya chini ya nyumba(substructure) na ile ya juu (superstructure). Katika hatua hii ni lazima kuhakikisha kuwa kuta zinanyooka na zina pimamaji. Ikumbukwe kuwa kuanzia kozi ya 2 hadi kwenye ring beam tofali hujengwa bila kutumia udongo saruji. Hata hivyo, kwa ajili ya kuongeza uimara udongo saruji laini (1:3) huwekwa kwenye kona, kwenye makato ya milango na madirisha. Kozi ya 2, kwa kuta za kugawa vyumba unaanza na tofali mbili za robo tatu ili kuondoa mfuatano wa maungio wima(straight vertical joints).
    Vipande vya nusu tofali hutumika zaidi kwenye makato ya madirisha na milango ili kuondoa mfuatano wa maungio wima.

 


Kutengeneza na kufunga boksi

    Utengenezaji wa box hufanyika kwa kuunganisha kwanza mbao za pembeni, kwa kutumia vibao maalum na kisha kulipachika ukutani na kuunganishwa na mbao za sahani kwa kutumia misumari. Box ni lazima liimarishwe vizuri pamoja na kuweka mirunda sehemu zote stahiki ili kuzuia kupinda au kuyumba kwa box hilo wakati wa kuweka zege.

 
   Ujenzi wa matofali mfereji (channel blocks)

    Hii ni teknolojia ambayo hupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mbao/miti kama vifaa vya kutengeneza kalibu ya kushika zege laini, ambapo matofali yenye umbo la kalibu hujengwa juu ya mstari wa mwisho kabla ya linta kwa lengo la kupokea zege laini. Kwa kuwa matofali hayo hufanana na tofali nyingine huficha eneo lenye linta na kufanya nyumba ionekane vizuri (Disappearing formwork).
    Hapa matumizi ya mbao za sahani na mirunda ni kwenye madirisha, milango na maeneo mengine yaliyo wazi, ambapo kuna linta. Njia hii ni bora, rahisi na rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya miti/mbao.
 


Kumwaga zege la linta
    Kabla ya kumwaga zege ni bora kufanya yafuatayo kwanza; kuweka nondo, kuweka nyaya za kufungia wall plates na kuweka mabomba ya umeme (conduit pipe) kwa nyumba yenye huduma ya umeme. Pia vipande vya mbao vyaweza kutumika kuweka matundu kwenye zege na kuvitoa zege likishanyauka kwa ajili ya kupitisha bomba za umeme pale ambapo kazi ya umeme itafanyika baadae na si lazima kununua bomba kipindi hicho kazi ya kumwaga zege ni kama inavyofanyika kwenye ujenzi wa kawaida isipokuwa tu, ni lazima kuhakiki kuwa mabomba ya umeme yako wima.
Ujenzi wa tofali juu ya linta
    Kozi ya kwanza baada ya linta, udongo mwashi hutumika ili kuunganisha linta na ukuta wa juu. Pia kulingana na ramani ukuta wa hanamu (gable) hujengwa baada ya kukamilika kwa hizo kozi 4. Ni muhimu matundu ya tofali kwa kuta zilizopo juu ya linta yajazwe udongo saruji laini.

 
 

Thursday 5 May 2016

UJENZI WA NYUMBA KWA KUTUMIA MATOFALI YA KUFUNGAMANA (INTERLOCKING BRICKS)


Ujenzi wa nyumba kwa kutumia matofali ya kufungamana ni mojawapo ya aina ya ujenzi wa gharama nafuu ambao huondoa matumizi ya udongo mwashi kama kiunganishi kati ya tofali na tofali ingawa mambo yote ya msingi na kanuni za ujenzi lazima vizingatiwe.
Kabla ya kuanza ujenzi ni lazima kuwe na msingi imara uliojengwa kwa vifaa imara ambao upo kwenye vipimo sahihi, ili kuweza kutumia tofali hizi. Sehemu ya msingi wa nyumba (substructure) itakuwa na-:

      Kitako cha msingi: zege/mawe
      Ukuta wa msingi: Matofali ya saruji na mchanga, udongo na saruji yanayofungamana, mawe au matofali ya kuchoma.
 
Endapo tofali za udongo-saruji za kufungamana zitatumika ni lazima unene wa ukuta wa msingi usipungue sm 30 (urefu wa tofali). Ili kukabiliana na hali ya unyevunyevu ni vyema kuimarisha zaidi tofali kwa kuongeza kiwango cha saruji kwenye udongo wakati wa ufyatuaji.
Ujenzi kwa kutumia matofali ya udongo au udongo ulioimarishwa umeonekana kuwa wa gharama nafuu zaidi kutokana na upatikanaji wa udongo katika sehemu kubwa nchini.
 
Katika ujenzi huu tofali linalotumika huwa na vipimo vifuatvyo:

      Urefu 300mm
      Upana 150mm
      Unene 100mm

Vilevile kuna vipande vya nusu na robo tatu tofali.
 
Tofali Zima
 

Robotatu tofali
 
Nusu tofali
 
Tofali Zima
 
Robotatu tofali mbili

Tofali la chaneli
 
Kabla ya kuanza ujenzi ni lazima kupitia ramani iliyopo ili kuona kama inakubaliana na vipimo vya urefu wa ukuta ambapo ni lazima vigawanyike kwa  tofali zima au nusu (yaani 300 au 150mm).

Mfano ukuta wenye urefu wa mita 3, hujengwa kwa tofali nzima 10, katika mstari mmoja wenye urefu huo. Ikumbukwe kuwa katika ujenzi huu hatukati vipande vyenye urefu mbalimbali kama ambavyo hufanyika katika ujenzi wa matofali yasiyofungamana, badala yake vipande vya nusu na robo tatu hutumika.
Nyumba imegawanyika katika sehemu kuu mbili:-

      Msingi:        Sehemu ya chini ya nyumba (substructure)
      Boma:         sehemu ya juu ya msingi
Msingi:       Msingi wa nyumba hujengwa kwa:

      zege,
      mawe
      matofali ya saruji na mchanga
      matofali ya udongo na saruji.

Namna ya kuset matofali ya kufungamana kwenye msingi uliojengwa kwa matofali ya saruji na mchanga.

Kwa kuwa msingi ndio sehemu inayobeba mzigo wa jengo zima ni muhimu vifaa vinavyotumika kuujenga viwe bora na imara. Kwa maeneo yaliyo mengi nchini zege, mawe na tofali za saruji mchanga ndio hutumika kujenga msingi wa nyumba. Hata hivyo matumizi ya udongo na saruji hutumika kujenga misingi kwa maeneo yenye udongo imara. Lakini mchanganyiko wake ni lazima uboreshwe zaidi ili kupata tofali imara lenye uwezo wa kubeba uzito na kuhimili hali ya unyevunyevu.

Boma: Sehemu hii ya nyumba hujengwa kwa kutumia zege, mawe, matofali ya mchanga na saruji, matofali ya udongo na saruji, matofali ya udongo na chokaa au matofali ya udongo. Ujenzi kwa kutumia matofali ya udongo au udongo ulioimarishwa umeonekana kuwa wa gharama nafuu zaidi ukilingnisha na ujenzi wa matofali ya saruji na mchanga. (itaendelea toleo lijalo)

Boma lililojengwa kwa kutumia matofali ya kufungmana
Usikose mwendelezo wa mfunzo haya, tukutane toleo lijalo.......