Monday, 31 October 2016

BAADHI YA MAJIBU YA MASWALI AMBAYO WATU WENGI WAMEKUWA WAKIJIULIZA

Swali: Bei ya mashine ya vigae ni kiasi gani?
Jibu: Tshs 250,000/=
 
Swali: Bei ya mashine ya matofali ya kufungamana ni kiasi gani?
Jibu: Tshs 650,000/=
 
Swali: Kama moja ya kazi ya matundu ni kupitisha mabomba ya umeme na kuimarisha kwa kumwaga rojorojo ya saruji katika kuta za kona ya jengo, kwenye madirisha na kwenye milango, Je wakati wa kumwaga zege ya lenta zege inayomiminwa si itaishia kwenye matundu?
Jibu: Nondo zinazowekwa kwenye lenta zinazuia umwagikaji wa zege inayomiminwa.
 
Swali: Kwanini isitengenezwe mashine inayotumia umeme ama Hydraulic?
Jibu: Gharama itakua kubwa sana na hivyo itaondoa unafuu wa utengenezaji tofali
 
Swali: Je kuna haja ya kupiga lipu kwenye nyumba iliyojengwa kwa kutumia matofali ya kufungamana?
Jibu: Haina lazima hasa nje. Kwa ndani ni muhimu ili kupata finishing nzuri
 
Swali: Je nyumba hizi zinadumu miaka mingapi?
Jibu: Zaidi ya miaka 45
 
Swali:Uimara wa nyumba zilizojengwa kwa kutumia teknolojia ya NHBRA ni upi.
Jibu: Sawa na uimara wa tofali za block
 
Swali: Kwanini mashine ya vigae isitumie umeme badala ya betri ya gari?
Jibu: Hii huiwezesha mashine kutumika sehemu yoyote hata isiyo na umeme (vijijini) ambako ndio kuna walengwa wakubwa.
 
Swali: Kwanini mashine ya matofali isitumie umeme ili kuwezesha kufyatua tofali nyingi kwa muda mchache?
Jibu: Inawezekana lakini Wakala unawalenga watu wa kipato cha kati na chini ili waweze kujenga nyumba bora za gharama nafuu. Mashine ya umeme itakua na gharama kubwa.
 
Swali:Kwanini vigae vinalowekwa maji?
Jibu: Kufanya viwe imara
 
Swali: Kwanini matofali yanamwagiliwa maji?
Jibu: Kufanya tofali kuwa imara
 
Swali: Kama eneo langu halina udongo mfinyanzi mwekundu, nitapata wapi udongo mwekundu?
Jibu: Sio lazima uwe udongo mwekundu, kinachohitajika ni udongo wowote mradi uwe na mfinyanzi wa kadiri ya asilimia 10 mpaka 40.
 
Swali: Kwanini matofali ya kufungamana yana matobo?
Jibu: Inapunguza uzito na inasaidia kubalansi hali ya hewa. Vile vile matobo haya yanatumika kupitisha nyaya za umeme
 
Swali: Kwanini matofali yajengwe bila udongo mwashi (mortar)? Je nyumba hiyo itakuwa imara kweli?
Jibu: Hiyo ndio aina ya tofali na teknolojia yake. Kuta za nyumba zinaimarishwa kwa nyumba kuwekwa lenta. Vilevile loki za kwenye tofali zinasaidia kuimarisha uimara wa nyumba.
 
Swali: Kwasababu gani tutumie udongo na saruji katika kufyatua matofali ya interlock na isiwe mchanga?
Jibu: Mchanga hauwezi kushikana bali udongo unashikamana ukishindiliwa kutokana na mfumo wa mashine yetu (tofali bila kibao). Vile vile mchanga hauna asili ya mfinyanzi ila udongo una asili ya mfinyanzi
 
Swali: Uzito wa vigae vya NHBRA ni kilo ngapi kwa kimoja.
Jibu: Kilo 2.6
 
Swali: Vigae vingapi vitatumika kuezeka nyumba ya vyumba vinne.
Jibu: Vigae 1700 kutegemea aina ya mchoro wa nyumba
Ni matumaini yangu tumejibu baadhi ya maswali kama kuna swali lingine au pendekezo usisite kutuandikia......

Thursday, 20 October 2016

TAARIFA ZA TAFITI

Nhbra Tanzania, hutoa taarifa mbalimbali za tafiti hususani zile zinazolenga teknolojia ya ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu kwa kupitia tovuti http://www.nhbra.go.tz/publications/5

Tuesday, 11 October 2016

MAABARA YA UPIMAJI VIFAA VYA UJENZI

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa Vya Ujenzi Nhbra Tanzania, una Maabara ambayo inafanya majaribio mbalimbali ya upimaji ubora na uimara wa vifaaa vya ujenzi.
Kupata ufafanuzi zaidi juu ya vipimo mbalimbali vya vifaa vya ujenzi na bei zake fika Ofisini kwetu Mwenge, Dar es Salaam muda ni kunzia saa 0730-1530hrs Jumatatu - Ijumaa au tembelea tovuti yetu
http://www.nhbra.go.tz/projects/22


Fundi Sanifu akipima uwezo wa udongo kubeba mzigo "load carrying capacity" kwa kutumia mashine ya Direct Shear katika Maabara ya NHBRA


Tuesday, 4 October 2016

SIKU YA MAKAZI DUNIANI

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila Mwaka ambapo kwa mwaka 2016 maadhimsho hayo yalifanyika tarehe 3/10/2016 kwenye viwanja vya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu "Nyumba Kitovu cha Miji" yaliongozwa na Mhe. William Lukuvi ambaye ni Waziri wa Wizara hiyo. Katika maadhimisho hayo Wakala wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi ulipata nafasi ya kushiriki maadhimisho hayo kama mdau wa usambazaji wa teknnolojia ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa kutumia tafiti mbalimbali ili kumnufaisha Mtanzania.
Arch. Godfrey Munyaga wa pili kulia akifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kwenye maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani 
Mhe. William Lukuvi akiangalia bango linaloonyesha baadhi ya kazi zilizokwisha fanywa na Wakala wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi, wengine ni Afisa Masoko wa Wakala Bi. Zubeda Salum pamoja na mwakilishi wa Shirika la Nyumba (NHC) 
Mhe. William Lukuvi akipata ufafanuzi juu ya shughuli za Wakala kutoka kwa Bw. Frimin Lyakurwa ambaye ni Msaidizi Mwandamizi wa Maktaba.

Monday, 9 May 2016

IJUE MAABARA YA KUPIMA VIFAA VYA UJENZI YA NHBRA

Maabara ya NHBRA imegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni:
  • Wet laboratory
  • Dry laboratory
Lengo la kupima ubora au uimara wa vifaa vya ujenzi au kufanya majaribio mbalimbali katika maabara ni kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika kwa ujenzi vinafikia kiwango cha chini cha ubora unaohitajika (minimum quality/strength requirement) kilichowekwa.


Oven
MAJARIBIO MBALIMBALI:

Majaribio ya udongo (soil test)
  • Kupambanua aina za udongo (soil classification)
  • Kushindilia (compaction related tests)
  • Upitishji maji na Uimara (compressibility, permeability and durability tests)
  • Jaribio la eneo la kazi (in-situ tests)
  • Shear strength tests
  • 
    Mashine ya kupima uimara wa udongo
Matofali na zege (blocks, bricks and concrete)
  • Mkandamizo (compressive strength)
  • Mchanganyiko (concrete mix design)
  • Kunyonya maji (absorption test)
  • Rebound hammer
  • Slump test
  • 
    Mashine ya kupima uimara wa zege na matofali
Aggregates
  • Kusagika (aggregates crushing value)
  • Kupondeka (aggregates impact value)
  • Kunyonya maji (water absorption)
  • Uimara kwenye msuguano (Los Angels abrasion value)
  • Uzito (bulk density)
  • Mabaki ya mimea (organic impurities)
Nondo
  • Kuvutika (Tensile strength)
  • Kukunjika (bending test)
  • Kukunjuka/kukunjua (rebending test)
Mbao (timber)
  • Unyevunyevu (moisture content)
  • Kukunjika (bending test)
Nachukua nafasi hii kuwakaribisha nyote kutumia maabara hii ambayo imesheheni na vifaa vya kisasa kwa vipimo na majaribio mbalimbali ya masuala ya ujenzi. nyote mnakaribishwa.

Saturday, 7 May 2016

UJENZI WA NYUMBA KWA KUTUMIA MATOFALI YANAYOFUNGAMANA (INTERLOCKING BLOCKS)


 Mwendelezo wa toleo lililopita.............
Ujenzi wa nyumba umegawanyika katika hatua zifuatazo: -

•      Kupima msingi wa jengo
 
   
•      Kuchimba msingi
•      Kumwaga zege la msingi
•      Kujenga kuta za msingi
•      Kuweka kifusi na kushindilia
•      Kupanga mawe
•      Kumwaga zege la jamvi
•      Kujenga kuta za boma
•      Kumwaga zege la linta
•      Kujenga juu ya linta
•      Kupaua jengo
•      Kuweka milango na madirisha
•      Kazi za umaliziaji na kazi za huduma mbalimbali mfano; umeme, maji, simu n.k
 
Ujenzi wa ukuta wa msingi

•     Ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu wakati wa utengenezaji wa tofali za msingi kuhusu uchanganyaji wa udongo na saruji. Vipimo vya unene vya ukuta wa msingi na kina hutegemea na aina ya jengo na sifa za udongo uliopo, inashauriwa kina kisiwe chini ya sentimeta 45 na unene wa ukuta wa msingi usiwe chini ya sentimeta 30 (urefu wa tofali moja).


 
Kuseti kuta za boma
•     Hatua inayofuata ni kuseti kuta za boma kwa kutumia ramani iliyopo. Hatua hii hufanyika kwa namna mbili: kwanza ni kuyapanga matofali kwa kuzingatia vipimo vya urefu wa kuta na kuondoa tofali maeneo yote ya uwazi kama milango na maeneo ya wazi ambayo yana mwendelezo wa ujenzi baada ya linta. Vipande robo tatu tofali hutumika wakati wa kugawa vyumba na kwenye maungio msalaba

 


Kujenga kuta za boma

•    Tofali huunganishwa kwa udongo mwashi kwenye kitako (bed jointing). Ni muhimu kutumia udongo mwashi kwenye kozi ya kwanza ili kuweka muunganiko kati ya sehemu ya chini ya nyumba(substructure) na ile ya juu (superstructure). Katika hatua hii ni lazima kuhakikisha kuwa kuta zinanyooka na zina pimamaji. Ikumbukwe kuwa kuanzia kozi ya 2 hadi kwenye ring beam tofali hujengwa bila kutumia udongo saruji. Hata hivyo, kwa ajili ya kuongeza uimara udongo saruji laini (1:3) huwekwa kwenye kona, kwenye makato ya milango na madirisha. Kozi ya 2, kwa kuta za kugawa vyumba unaanza na tofali mbili za robo tatu ili kuondoa mfuatano wa maungio wima(straight vertical joints).
•    Vipande vya nusu tofali hutumika zaidi kwenye makato ya madirisha na milango ili kuondoa mfuatano wa maungio wima.

 


Kutengeneza na kufunga boksi

•    Utengenezaji wa box hufanyika kwa kuunganisha kwanza mbao za pembeni, kwa kutumia vibao maalum na kisha kulipachika ukutani na kuunganishwa na mbao za sahani kwa kutumia misumari. Box ni lazima liimarishwe vizuri pamoja na kuweka mirunda sehemu zote stahiki ili kuzuia kupinda au kuyumba kwa box hilo wakati wa kuweka zege.

 
   Ujenzi wa matofali mfereji (channel blocks)

•    Hii ni teknolojia ambayo hupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mbao/miti kama vifaa vya kutengeneza kalibu ya kushika zege laini, ambapo matofali yenye umbo la kalibu hujengwa juu ya mstari wa mwisho kabla ya linta kwa lengo la kupokea zege laini. Kwa kuwa matofali hayo hufanana na tofali nyingine huficha eneo lenye linta na kufanya nyumba ionekane vizuri (Disappearing formwork).
•    Hapa matumizi ya mbao za sahani na mirunda ni kwenye madirisha, milango na maeneo mengine yaliyo wazi, ambapo kuna linta. Njia hii ni bora, rahisi na rafiki kwa mazingira kwani hupunguza matumizi ya miti/mbao.
 


Kumwaga zege la linta
•    Kabla ya kumwaga zege ni bora kufanya yafuatayo kwanza; kuweka nondo, kuweka nyaya za kufungia wall plates na kuweka mabomba ya umeme (conduit pipe) kwa nyumba yenye huduma ya umeme. Pia vipande vya mbao vyaweza kutumika kuweka matundu kwenye zege na kuvitoa zege likishanyauka kwa ajili ya kupitisha bomba za umeme pale ambapo kazi ya umeme itafanyika baadae na si lazima kununua bomba kipindi hicho kazi ya kumwaga zege ni kama inavyofanyika kwenye ujenzi wa kawaida isipokuwa tu, ni lazima kuhakiki kuwa mabomba ya umeme yako wima.
Ujenzi wa tofali juu ya linta
•    Kozi ya kwanza baada ya linta, udongo mwashi hutumika ili kuunganisha linta na ukuta wa juu. Pia kulingana na ramani ukuta wa hanamu (gable) hujengwa baada ya kukamilika kwa hizo kozi 4. Ni muhimu matundu ya tofali kwa kuta zilizopo juu ya linta yajazwe udongo saruji laini.

 
 

Thursday, 5 May 2016

UJENZI WA NYUMBA KWA KUTUMIA MATOFALI YA KUFUNGAMANA (INTERLOCKING BRICKS)


Ujenzi wa nyumba kwa kutumia matofali ya kufungamana ni mojawapo ya aina ya ujenzi wa gharama nafuu ambao huondoa matumizi ya udongo mwashi kama kiunganishi kati ya tofali na tofali ingawa mambo yote ya msingi na kanuni za ujenzi lazima vizingatiwe.
Kabla ya kuanza ujenzi ni lazima kuwe na msingi imara uliojengwa kwa vifaa imara ambao upo kwenye vipimo sahihi, ili kuweza kutumia tofali hizi. Sehemu ya msingi wa nyumba (substructure) itakuwa na-:

•      Kitako cha msingi: zege/mawe
•      Ukuta wa msingi: Matofali ya saruji na mchanga, udongo na saruji yanayofungamana, mawe au matofali ya kuchoma.
 
Endapo tofali za udongo-saruji za kufungamana zitatumika ni lazima unene wa ukuta wa msingi usipungue sm 30 (urefu wa tofali). Ili kukabiliana na hali ya unyevunyevu ni vyema kuimarisha zaidi tofali kwa kuongeza kiwango cha saruji kwenye udongo wakati wa ufyatuaji.
Ujenzi kwa kutumia matofali ya udongo au udongo ulioimarishwa umeonekana kuwa wa gharama nafuu zaidi kutokana na upatikanaji wa udongo katika sehemu kubwa nchini.
 
Katika ujenzi huu tofali linalotumika huwa na vipimo vifuatvyo:

•      Urefu 300mm
•      Upana 150mm
•      Unene 100mm

Vilevile kuna vipande vya nusu na robo tatu tofali.
 
Tofali Zima
 

Robotatu tofali
 
Nusu tofali
 
Tofali Zima
 
Robotatu tofali mbili

Tofali la chaneli
 
Kabla ya kuanza ujenzi ni lazima kupitia ramani iliyopo ili kuona kama inakubaliana na vipimo vya urefu wa ukuta ambapo ni lazima vigawanyike kwa  tofali zima au nusu (yaani 300 au 150mm).

Mfano ukuta wenye urefu wa mita 3, hujengwa kwa tofali nzima 10, katika mstari mmoja wenye urefu huo. Ikumbukwe kuwa katika ujenzi huu hatukati vipande vyenye urefu mbalimbali kama ambavyo hufanyika katika ujenzi wa matofali yasiyofungamana, badala yake vipande vya nusu na robo tatu hutumika.
Nyumba imegawanyika katika sehemu kuu mbili:-

•      Msingi:        Sehemu ya chini ya nyumba (substructure)
•      Boma:         sehemu ya juu ya msingi
Msingi:       Msingi wa nyumba hujengwa kwa:

•      zege,
•      mawe
•      matofali ya saruji na mchanga
•      matofali ya udongo na saruji.

Namna ya kuset matofali ya kufungamana kwenye msingi uliojengwa kwa matofali ya saruji na mchanga.

Kwa kuwa msingi ndio sehemu inayobeba mzigo wa jengo zima ni muhimu vifaa vinavyotumika kuujenga viwe bora na imara. Kwa maeneo yaliyo mengi nchini zege, mawe na tofali za saruji mchanga ndio hutumika kujenga msingi wa nyumba. Hata hivyo matumizi ya udongo na saruji hutumika kujenga misingi kwa maeneo yenye udongo imara. Lakini mchanganyiko wake ni lazima uboreshwe zaidi ili kupata tofali imara lenye uwezo wa kubeba uzito na kuhimili hali ya unyevunyevu.

Boma: Sehemu hii ya nyumba hujengwa kwa kutumia zege, mawe, matofali ya mchanga na saruji, matofali ya udongo na saruji, matofali ya udongo na chokaa au matofali ya udongo. Ujenzi kwa kutumia matofali ya udongo au udongo ulioimarishwa umeonekana kuwa wa gharama nafuu zaidi ukilingnisha na ujenzi wa matofali ya saruji na mchanga. (itaendelea toleo lijalo)

Boma lililojengwa kwa kutumia matofali ya kufungmana
Usikose mwendelezo wa mfunzo haya, tukutane toleo lijalo.......