Saturday 25 July 2015

VIGAE MKONGE

Vigae Mkonge ni nini?

Ni aina mojawapo ya vigae vitumikavyo kuezekea nyumba. Vifaa vinavyotumika
kutenegeneza Vigae Mkonge ni Saruji, Mchanga, nyuzi za katani zitokanazo na zao la
mkonge na rangi. Nyuzi za mkonge hutumika ili kuongeza uimara wa vigae.
 
Kutokakana na utafiti uliofanywa na NHBRA imeonekana kuwa vigae mkonge ni mkombozi kwa
mtu wa kawaida hasa wa kipato cha wastani na cha chini kwa kuwa utengenezaji wake hutokana na
vifaa vipatikanavyo hapa nchini na huweza kutengenezwa na mtu mmoja mmoja, ama vikundi mahali
popote mijini na vijijini ili kuboresha makazi tofauti na vifaa vingine vya kuezekea ambavyo
vinapatikana viwandani kama mabati ya Aluminium, vigae vya viwandani na hata vile vitokavyo nje
ya nchi.
 
Utengenezaji wa Vigae Mkonge
 
Utengenezaji wa vigae mkonge ni lazima uwe na vifaa vifuatavyo: 
  • Mashine mtetemo (Vibrating Machine)
  • Saruji
  • Mchanga 
  • Nyuzi za katani
  • Rangi
  • Maji safi
  • Pasi mwashi
  • Mwiko mwashi
  • Kizoleo
  • Chepe 
  • Karai/beseni
 
 
Mashine mtetemo ya kutengenezea Vigae Mkonge
 
Nyuzi za katani zikiandaliwa, pembeni ni kalibu (moulds) za vigae

Hatua za utengenezaji

  • Changanya saruji na mchanga
  • Weka rangi
  • Weka nyuzi za mkonge kwa kiasi kinachohitajika
  • Ongeza maji katika mchanganyiko mkavu
  • Weka karatasi ya nailoni juu ya mashine na kukandamiza na fremu ya chuma
  • Jaza mchanganyiko ndani ya fremu ya chuma
  • Tetemesha mchanganyiko ulioko ndani ya fremu
  • Ondoa karatasi lenye mchanganyiko na kuweka juu ya kalibu iliyoandaliwa
  • Acha kigae juu ya kalibu si chini ya saa 12 baada ya hapo vigae lazima vizamishwe kwenye maji si chini ya siku 21 kwa ajili ya kuvikomaza.
 
 
Hatua mbalimbali za utengenezaji vigae huko Kasulu-Kigoma

 
Baada ya saa 18, vigae hutolewa katika kalibu na kuzamishwa majini kwa muda wa siku 28 kisha hutolewa na kuachwa vikauke kwa muda wa siku 7, baada ya hapo vigae vinakuwa tayari kwa kuezekea.

"Sink" la kukomazia vigae vya kuezekea
 
Vigae vikikaushwa tayari kwa matumizi


Faida za Vigae Mkonge

  • Vifaa vitumikavyo kutengenezea vigae hupatikana nchini
  • Utengenezaji ni rahisi hata kwa mtu asiyekuwa fundi
  • Hupendezesha jengo na kulifanya kuwa na thamani ya juu kwa gharama nafuu
  • Hupozesha joto/baridi na kelele za mvua
  • Vina uzito mdogo
  • Gharama nafuu
  • Hudumu kwa muda mrefu
Nyumba zilizoezekwa kwa vigae mkonge katika maeneo tofauti

Muungano Housing Co-operative-DSM
 
Mikocheni DSM
 
Chamazi DSM
 
Miyuji Dodoma
 
Ukonga DSM
 



 

 

Saturday 18 July 2015

UJENZI WA MATOFALI YA UDONGO SARUJI YA KUFUNGAMANA

Wakati wa ujenzi wa matofali haya hutumii udongo mwashi (mortar) kuyaunganisha kwa kuwa umbo lake linaruhusu kufungamana na kushikana bila tatizo lolote na ndio maana yanaitwa matofali ya kufungamana (interlocking Bricks) isipokuwa katika mstari wa kwanza kabisa chini unaoungana na msingi (foundation) ni lazima uweke udongo mwashi "mortar" ili kuweza kuunganisha ukuta na msingi ili uwe imara zaidi.

 

 
Ujenzi wa matofali ya kufungamana katika hatua za mwanzo huko Lufwisi Sikonge, Tabora


 
Kuanzia mstari (course) wa pili unaendelea kupanga matofali bila kuweka udongo mwashi lakini ukizingatia taratibu na masharti yote ya ujenzi hadi kwenye linta, kisha unafunga linta yako kama inavyotumika katika ujenzi wa aina nyingine ya matofali, au unaweza kutumia matofali ya chaneli ya linta (lintel channel) katika kufunga linta na kwa kutumia njia hii hautahitaji kufunga box la mbao kwa ajili ya linta isipokuwa matofali yenyewe yanachukua nafasi ya box la mbao hivyo kutohitajika matumizi ya mbao kwa ajili ya kufunga linta.

Linta ya box ilitumika katika ujenzi wa Ofisi ya Mbunge wa Manyoni-Singida

Muonekano wa Ofisi hiyo baada ya kuezekwa
 

Nyumba hizi zimefungwa linta kwa kutumia matofali ya linta chaneli huko Miyuji-Dodoma



Matofali ya kufungamana pia hutumika katika ujenzi wa uzio (fence) kama picha hapo chini zinavyoonyesha.

 
 
Nyumba hii na uzio wake iko Mikocheni B Dar es salaam


Mwananchi, hujachelewa bado wasiliana na NHBRA kupata huduma zao ili nawe uweze kumiliki nyumba, wasiliana nasi kwa simu namba +255 679 972 715 au dawatilamsaada@nhbra.go.tz

 

Friday 17 July 2015

UTENGENEZAJI WA MATOFALI YANAYOFUNGAMANA YA UDONGO SARUJI

Matofali haya yanatumia udongo na saruji katika utengenezaji wake ndio maana yanaitwa matofali ya udongo saruji. udongo wa aina zote unaweza kutumika kutengeneza matofali haya, lakini udongo unaofaa zaidi ni ule wenye kiasi cha mfinyanzi kati ya 10% hadi 40%. Udongo ukiwa na kiasi cha mfinyanzi chini ya 10% udongo huo haufai kutengeneza matofali haya kwani mnato unakuwa mdogo hivyo tofali halitashikamana, kutokana na aina ya mashine zinazotumika  tofali halitaweza kubebeka kutoka katika mashine kwa kuwa mashine inayotumika kutengeneza haitumii vibao kwa ajili ya kubebea. Kiasi cha mfinyanzi kikizidi 40% udongo huo unafaa kuchanganywa na saruji ila hushauriwi kufanya hivyo kwa sababu kiasi cha saruji kinachotumika ni kikubwa hivyo kukuongezea gharama za utengenezaji wa matofali hayo, tofali litanywea baada ya kukauka, hivyo kupasuka kwa sababu ya mfinyanzi kuwa mwingi, pia udongo huo hauwezi kuchanganyika vizuri na saruji kwa kutumia chepe kwa sababu ya mnato mkali au udongo wenye kiasi cha mfinyanzi zaidi ya asilimia arobaini unaweza kupiga matofali bila ya kuchanganya na saruji ila italazimika kuyachoma matofali hayo ili yawe imara zaidi.

 
Ili kujua kiasi cha mfinyanzi kilichopo katika udongo ili kujua kiasi cha saruji kinachohitajika katika kuchanganya na udongo wakati wa kutengeneza matofali yanayofungamana kuna majaribio yanayofanyika ili kuweza kujua hayo yote. majaribio hayo ni:
  1. jaribio la chupa (bottle test)
  2. jaribio la kasha (shrinkage box test)
JARIBIO LA CHUPA

Jaribio hili hutumika kupima kiasi cha mfinyanzi kilichopo katika udongo unaotaka kuutumia,Udongo unaotumika ni udongo wa chini udongo wa juu ni lazima uondolewe kwani ni udongo wenye mbolea na mizizi haufai kwa shughuli za ujenzi, udongo unaofaa ni ule wa chini hivyo ni lazima kuhakikisha kuwa udongo wote wenye mizizi na mbolea uneondolewa.


 
Picha za jaribio la chupa katika kutambua kiasi cha mfinyanzi katika udongo

 

JARIBIO LA KASHA

Jaribio hili hufanyika ili kujua uwiano wa kuchanganya udongo na saruji ili kuweza kutengeneza matofali yenye ubora unaotakiwa. Kasha linalotumika katika jaribio hili ni kam linavyoonekana katika picha hapo chini.
 
Jaribio likiwa limekamilika, matokeo yanapimwa
 
 
  • Baaada ya kupata majibu katika majaribio  na kupata uwiano wa kuchanganya saruji na udongo hatua za upimaji na uchanganyaji huanza.
  • Udongo uwe mkavu kabisa na kama una chembechembe kubwa udongo unaotumika lazima uchekechwe.
  • Tumia ndoo au karai kupima udongo.
  • Changanya udongo na saruji hadi vichanganyike vizuri
  • Nyunyizia maji hadi udongo uwe na uwezo wa kushikamana lakini usilowe hadi kutengeneza tope.
 
Udongo ukichanganywa na saruji tayari kwa kufyatua matofali.
Mashine ya kutengenezea matofali ni lazima ifungwe kwenye kitako cha mbao kwa kutumia bolt na
nut ili ikae itulie isisumbue wakati wa kufanya kazi ya ufyatuaji matofali pia ni lazima kuiwekea
vilainishi ili kupunguza msuguano wa vyuma wakati wa kufyatua matofali.
 


Hatua za ufyatuaji matofali
 
  • Funua mfuniko wa mashine
  • Jaza udongo kwenye kasha la mashine
  • Funika mfuniko
  • Shindilia
  • Funuo mfuniko
  • Kandamiza ili kutoa tofali kwenye mashine
  • Tofali hubebwa na mtu mmoja kwa mikono miwili na kulipeleka kuweka sehemu iliyoandaliwa
 
Umwagiliaji maji hufanyika kwa muda wa siku saba hadi ishirini na nane tangu yanapofyatuliwa

 
Matofali yakishakauka yanakuwa tayari kutumika katika ujenzi kama picha chini inavyoonyesha.




Jiwezeshe tukuwezeshe, kwa maelezo na huduma wasiliana nasi kwa simu namba +255 22 2771971 au info@nhbra.go.tz

Tuesday 7 July 2015

IJUE NHBRA

National Housing and Building Research Agency-NHBRA ni Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi. Ni wakala wa Serikali ambao ulianzishwa mwaka 2001. Wakala huu uko chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ukiwa na jukumu la kufanya utafiti wa vifaa vya ujenzi vipatikanavyo hapa nchini kwa lengo la kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba ili kuwawezesha wananchi kujenga nyumba bora na imara kwa gharama nafuu.

Katika kufanikisha ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu, NHBRA inashauri wananchi watumie teknolojia ya matofali ya kufungamana katika ujenzi wa nyumba zao kwani matofali haya yanatengenezwa kwa kutumia udongo na saruji kidogoili kuwezesha tofali kuwa imara zaidi. Matofali haya yanatengenezwa na mashine maalum ambayo itakuwezesha kutoa umbo la kufungamana kwa matofali ya aina mbalimbali ambayo hutumika katika ujenzi wa nyumba.


                                             Mashine za kufyatulia matofali ya kufungamana

inaaminika kwamba sehemu kubwa ya nchi yetu udongo unapatikana kwa wingi hivyo wananchi wakiweza kuzipata mashine hizi wataweza kufyatua matofali haya na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora na imara kwa gharama nafuu.

                                     Tofali hizi zimefyatuliwa huko Lukokoda wilayani Tandahimba

Tandahimba ina udongo unaofaa sana katika kutengeneza tofali hizi, wananchi wa Tandahimba jiwezeshe tukuwezeshe kumiliki nyumba bora na imara kwa gharama nafuu kabisa. kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu +255 22 2771971 au info@nhbra.go.tz vile vile unaweza kutoa maoni yako hapa karibuni sana